Tuesday, May 31

Mandhari

Kwa sasa tumetua uwanja wa ndege wa Mwanza, baada ya masaa kadhaa tutakua tunaelekea Kigoma. Picha hii inaonesha mandhari ya Uwanja wa Ndege, Safari yangu ndo imeanza, na siyo mbaya tukisafiri pamoja..... karibuni !!

Safari ya Kigoma

Niko Uwanja wa ndege wa Dar Es salaam nasubiri kwenda Kigoma. Ntakuwa huko kwa wiki nzima, naamini ntarejea najua kupika dagaa kwa style yao watu wa Kigoma. Ntashare nanyi mapishi hayo.
Naamini pia ntaweza kuona mapishi mengine mengi mazuri tu ndani ya Kigoma na kuwahabarisha maeneo yanapopatikana na namna ya kuyapika.
Karibuni Kigoma!!!!!!

Monday, May 30

Menyu toka kwa Rafiq

Nafurahi kupata email zinazotoka kwa marafiq mbalimbali, ambapo wanaamua kushare nasi menyu yao, na naamini kuna marafiq ambao wataleta mapishi yao namna wanavyopika menyu mbalimbali.
Kutoka kwa rafiq ambaye hakuacha jina lake, alinitumia picha ya chakula alichokula jana hakuweka wazi kama ni cha mchana au usiku, ila alichosema ni kwamba anapenda sana kuku.


Asante sana Rafiq, na naamini menyu ilikua tamu sana!

Sunday, May 29

Nipo Kinondoni bado

Leo nilipigiwa simu na rafiq yangu Janeth ambaye alivutiwa na menyu ya tarehe 23, kitimoto ya Kinondoni. , baada ya kuona picha ya ile menyu alipatwa na hamu ya kwenda kuijaribu. Baada ya kumuelekeza vyema na kumpatia namba ya kaka alimpigia simu na kuweka oda ya kutosha jamii aliyokua nayo. Jumla walikua watu kama saba, na hizi ni picha alizonitumia.

Walimuomba mpishi awapikie Kitimoto ya aina yeyote itakayowafurahisha, na baada ya nusu saa, kaka alirejea na sahani mezani. Aliwapikia Makange ya Kitimoto.


Janeth anasema kuwa katika muda wa chini ya dakika kumi, kimya kilitanda mezani na hali ilibadilika na kilo 2 zilizowekwa mezani zilitoweka. Ghafla sahani ilibakia hivi:

Sahani ya pembeni kama vile chumvi na pilipili havijaguswa...... Ila inaonesha jinsi gani walifurahia chakula kilichotayarishwa kwa ajili yao.
Asante Janeth kwa habari na picha.

Wednesday, May 25

Lunch ya leo - Mtori

   Tumezoea kuunywa Mtori kwenye bar au hotels, mida ya asubuhi kama kifungua kinywa, tukishushia na chapati au andazi.
   Leo nyumbani mama ameamua kupika kama Lunch. Kwenye picha unaonekana mtamu.... Nakuhakikishia ni mtamu.
    Kujifunza namna ya kupika mtori (Orijino) nikimaanisha ule ambao unapikwa Rombo, Moshi basi karibu kwenye  Mapishi time
 
 
   Kama nilivyoelekezwa na mama, nami nakuelekeza. Ukifanikiwa kupika nijulishe, na kama utaweza piga na picha nitumie kupitia menutimes@gmail.com

Tuesday, May 24

Usiku wa leo - Rosti ya Maini & Chapati

Tena nimeingia jikoni kuweka mkono wangu katika mapishi ya usiku wa leo. Niliamua kupika Rosti ya Maini na Chapati. Kwa kujua nimelipikaje rosti hilo tafadhali angalia Mapishi time. Chapati ni kwa hisani ya Bakhresa, zapatikana kwenye Supermarkets nyingi tu mjini hapa, hivyo nilifanya kuzikaanga tu.
Karibuni...
 

Monday, May 23

Kitimoto ya Kinondoni

Katika pitapita yangu mitaa ya Kinondoni, kama unatokea Salenda baada ya makaburi kona ya kwanza kushoto kama unaenda Bar ya Bamboo, mbele ya gereji upande wa kushoto kuna contena mbili. Ukifika pale tafuta sehemu ya kuegesha gari kama una usafiri, halafu ingia hapo Ulizia ya Kuchoma.
Huyu jamaa sijui anaichomaje ila ikifika saa 12 na dakika kadhaa jioni, mzigo wote unakua umeisha. Sijajua kwa siku anauza kilo ngapi. Unaweza kuweka oda yako mapema kwa kumpigia simu namba 0754 228 502, halafu unaongea na Ellia unamwelezea mahitaji yako , baada ya muda unafika na kupata oda yako safi inakusubiri.
huu ni mfano tu wa ya kuchoma, ila kuna ya rosti na aina kadhaa za upishi.

Sijawahi kujua kwanini huwa chumvi inawekwa nyingi sana pale mteja anapoagiza chakula, ntatafuta sababu ni nini haswa halafu ntakuhadithia.


Sunday, May 22

Mapishi ya keki

Leo tutaangalia namna ya kupika keki ya Chokoleti.
Kuna urahisi kwenye namna ya kupika endapo utanunua unga ambao tayari umechanganywa na michanganyiko kadhaa tayari kwa kupika keki, na unachohitaji kufanya ni kuongeza baadhi ya viungo kidogo kisha kuiweka kwenye jiko la Oven tayari kwa kuoka.

Mahitaji:
  • Unga uliyotayarishwa tayari kwa kupikwa (pakiti moja - 500g)
  • Mayai matatu
  • Mafuta ya kupikia 80ml
  • Maji safi 200ml
  • Butter kiasi
Kwa ajili ya topping
  • Nunua chokolate yenye karanga
  • Maziwa kikombe kimoja



  • Hatua za kupika:

  • Tayarisha oven yako kwa kuiwasha katika moto wa nyuzi 185 sentigrade (365F)
  • Paka butter kiasi kwenye kikaangio chako kisha kiweke pembeni
  • Koroga mayai, changanya na maji safi, mafuta ya kupikia pamoja na unga uliyotayarishwa mpaka vichanganyike vyema
  • Nyunyuzia unga wa cocoa au unga wa ngano katika kikaangio chako ulichokipaka butter
  • Weka mchanganyiko wa unga, mayai, mafuta ya kupikia pamoja na maji safi ndani ya kikaangio chako
  • Ingiza ndani ya oven na funga mlango uache keki iive kwa dakika zitegemeazo aina ya kikaangio chako.
  • (Iwapo kikaangio chako ni shepu ya mstatili na kina vipimo hivi: 5 X 33 X 22cms = 2 X 13 X 9 inches basi utatumia muda wa dk 40 - 45 kupika keki yako).
  • (Iwapo kikaangio chako ni shepu ya duara na kina vipimo hivi: 22cms = 9 inches basi utatumia muda wa dk 40 - 45 kupika keki yako).
  • (Iwapo kikaangio chako ni shepu ya duara na kina vipimo hivi: 15cms = 6 inches basi utatumia muda wa dk 55 - 60 kupika keki yako).
  • Tumia toothpick au kijiti cha mbao kisafi kuchomeka katikati ya keki yako kuangalia kama imeiva vyema, baada ya hizo dakika hapo juu kupita
  • Iwapo kijiti cha mbao/ toothpick kitatoka bila ya ungaunga basi keki yako imeiva vyema, iepue na uzime jiko
  • Iwapo kijiti cha mbao/ toothpick kitatoka na unga unga basi ujue bado keki yako haijaiva vyema. Funga mlango na uache iive kwa muda. Hakikisha kijiti kinatoka bila ya unga unga
  • Iache keki yako ipoe kwa dakika 15 - 20 kabla hujaiondoa kwenye kikaangio
Namna ya kutengeneza topping:
  • Weka sufuria safi kwenye jiko
  • Vunja vunja chokolate yako na iweke kwenye sufuria yenye moto
  • Ongeza maziwa kikombe kimoja yenye moto
  • Koroga mchanganyiko huo mpaka uchanganyike vyema
  • Epua mchanganyiko wako weka na anza kupaka kwa kutumia brashi kwenye keki yako ambayo itakua imeshapoa
  • Keki yako ipo tayari kwa kuliwa
Waweza kula na soda, chai, juice, maji, maziwa au hata peke yake. 
                      
       
Karibuni !!

Thursday, May 19

Menyu ya Kitaani

Kinondoni, kona ya Best bite pale, nenda mbele kona ya kwanza kulia achana nayo, nenda mbele kona ya pili ingia, nenda mbele utakutana na gereji ya mabenz, wasalimie ndugu zetu kisha endelea mbele kidogo upande wa kulia utakuta kuna baa nzuri tu.
Sifa kubwa kuna bwawa la maji pale kwahiyo mbu ndo nyumbani kwao, lakini sio neno wanapigwa dawa mara kwa mara.
Hii sehemu inasifika sana kwa kupika nyama ya maana, namaanisha kuchoma nyama ya maana ya Ng'ombe na mwenzie Mbuzi. Sijajua wanaweka nini wakati wa kumarinate ila ni laini yaani kama inateleza flani mdomoni halafu ni tamu mno.
Hili ni moja ya jiko lao, nadhani wanayo kama matatu au manne.
 
 
Sasa hii ni mbuzi ya Tsh 8,000/= kaka alikua ananikatia, mie mwenzenu mgonjwa wa nyama choma yeuwiiiiiii
 
Halafu pembeni kuna chipsi zimekaushwa uzuri mno......


Baada ya ile nyama kukatwa na mchuzi wake huwa inaonekana hiviiiii, kama wataka kufungiwa ukalie kwingine, na sio pale pale.

Kama upo Dar Es Salaama na hujawahi patembelea hapa, nakusihi uende. Kama upo mkoa au nchi nyingine, siku ukija Dar fanya juu chini usiache pitia hapa upate utamu, au tuma rafiki kama utakua busy sana.
Nakutakia mchana mwema na Siku njema!!!!


Wednesday, May 11

Mapishi ya wali wa nazi, viazi na samaki kaanga

   Leo tunapika wali wa nazi, viazi vya kukaanga, mchemsho wa mboga za majani na samaki za kukaanga.

Mahitaji:
  • Mchele
  • Tui la nazi
  • Chumvi
  • Viazi
  • Kitunguu maji
  • Zucchin
  • karoti
  • French beans
  • Samaki
  • Tangawizi
  • Vinegar
  • Ndimu
  • Pilipili manga
  • Mafuta ya kupikia.
Hatua za kupika:
Tuanze na wali wa nazi
  • Tayarisha maji yenye tui la nazi na chumvi kidogo na uweke kwenye moto
  • Osha mchele tayari kwa kupikwa
  • Kabla maji hayajachemka, na yakiwa yamepata moto sana, ingiza mchele uliyo oshwa ndani ya sufuria
  • Pika wali katika moto mdogo hadi uive

  • Epua wali wako tayari kwa kuliwa.
Tuje kwenye viazi vya kukaanga
  • Menya maganda ya viazi
  • Osha viazi tayari kwa kupikwa
  • Weka viazi ndani ya sufuria yenye maji, chumvi kidogo na vitunguu tayari kwa kuchemshwa
  • Chemsha viazi kiasi
  • Epua viazi vyako na chuja maji uliyochemshia


  • Chukua kikaangio na weka mafuta ya kupikia
  • Kaanga viazi vyako mpaka vibadilike rangi ya brown na kuiva vyema
  • Epua viazi vvyako tayari kwa kuliwa.
Tupike mboga zetu
  • Chukua zucchini, karoti, french beans na giligilani


  • Katakata vipande vilivyo sawa
  • Viweke ndani ya sufuria na maji kiasi na chumvi kiasi


  • Chemsha kiasi na hakikisha visiive sana.
Tumalizie na Samaki za kukaanga
  • Safisha samaki vyema
  • Katakata vitunguu swaumu na tangawizi na kisha viponde
  • Katakata samaki kisha vichane kidogo kidogona kisu kuruhusu mchanganyiko uingie ndani ya samaki
  • Changanya Vitunguu swaumu na tangawizi vilivyopondwa na ndimu, mafuta ya kupika, vinegar pamoja na vipande vya samaki

  • Acha mchanganyiko huo uingie ndani ya vipande vya samaki kwa muda wa dk 30 - 45
  • Weka mafuta ya kupikia ndani ya kikaango na yaache yapate moto wa kutosha
  • Ingiza vipande vya samaki ndani ya mafuta na kaanga mpaka vipate rangi ya brown na viive kabisa
  • Epua samaki wako tayari kwa kuliwa.
Naamini, umejifunza vyema..... waweza kutuma mapishi yako kupitia menutimes@gmail.com
au kama una picha ya chakula ungependa iwekwe basi tuma kupitia anuani hiyo.
Karibuni.

Usafi wa mazingira ya Upishi

   Chakula ni kitu ambacho kinapaswa kutengenezwa na kuhifadhiwa kwenye sehemu yenye usafi wa hali ya juu na muonekano wa kuvutia na mzuri.
   Binafsi Coco beach tunaponunua mihogo na viazi, eneo lake halijaniridhisha kwa kweli. Nahisi kama wangeweza kupatengeneza vyema zaidi. Labda wangeweka mabati au makuti kujikinga na mvua na jua, wengekuwa na mapipa ya maji kuhifadhi maji mengi kwa usalama, na meza kubwa kutosha kuweka bidhaa zao, naamini kama pangekua pana muonekano mzuri zaidi.

   Hivi ndivyo panavyoonekana kwa sasa, toa ushauri wako Je, pana hitaji kuboreshwa? au tuendelee tu? Karibu...

Mihogo ya Coco beach

Dar pazuri sana, katika kila aina ya chakula, kuna pahala pake ambapo wengi wetu wanapajua ndio chakula flani kinapatikana hapo, tena kwa utamu wa ajabu. Iwe kitaani au mgahawani na hata kwa nyumba ya flani.
Ukiulizia Dar wapi waweza pata crisps za mihogo na viazi fresh, ukagusia mihogo na viazi vitamu vya kukaanga, katika sehemu zitakazotajwa nina hakika Coco beach itakuwepo, almaarufu kwa Bonge.
Mchana wa leo nimepita pale, si unajua hamu tu ilinipata na kitambo sijatembele pale. kwa shilingi 1,000/=  za kitanzania niliweza pata mhogo mmoja na kiazi kimoja na chachandu yake (kachumbari si mpenzi sana hivyo nikasahau hiyo).

 
Nkashushia na maji bariiiidi, nikageuza zangu. Hii ndio sahani yangu nikiwa ndani ya gari. Karibu...

Tuesday, May 10

Menyu ya Usiku

   Usiku wa leo, niliingia jikoni mwenyewe na kuandaa menyu ya leo. Nilipika viazi watoto a.k.a baby potatoes, wali wa nazi, vegetable rosti, kuku wa kukaanga na mchemsho wa mboga za majani.
 
 
   Namna ya upikaji wake nifuate kwenye mapishi nikuhadidhie. binafsi nlishushia na juisi ya maembe.... Karibu!!

Monday, May 9

Ujumbe wa Wiki

ATTITUDE:
If you have a positive attitude towards life, everything else will follow.

Sunday, May 8

Menyu ya nyumbani - Siku ya Mama.

   Jumapili tulivu Dar Es Salaam, baada ya kukimbizana na Moshi, nipo home na leo menyu iliyopikwa kwetu ni hii. Wali wa nazi, Maharagwe yenye karanga, Samaki wa kukaanga na kachumbari (kachumbari iliyotengenezwa ni vitunguu maji, nyanya, chumvi kwa mbali na ndimu). Shukrani kwa kaka yangu kwa kukaanga samaki baada ya kuwamarinate, Bi mkubwa aliweka mkono kwenye wali na maharagwe..... lovely.
 
 
Nitumie leo Siku ya Mama wewe umekula nini, halafu tutashare na wenzetu humu ndani. Karibuni!!

Friday, May 6

Pizza ya Moshi

   Mchana wa jana nilipata lunch yangu Hotel ya Leopard iliyoko Moshi mjini kabisa. Kwa ukaribisho wa rafiki yangu Primo, niliweza kupata Pizza ambayo chaguo lake nililiongezea vikorombwezo. Orijino inaitwa "Trilly Extra Chicken and Beef". Niliomba kuongezewa nanasi na extra nyama.
 
 
Ukifika Moshi na kama wewe ni mpenzi wa Pizza, na wataka kula Pizza tamu basi pitia hapa Leopard Hotel, wana menu ya maana.

Thursday, May 5

Mkoa wa Kilimanjaro

Mkoa wa Kilimanjaro umeundwa na wilaya 6 ambazo ni Rombo, Hai, Siha, Same, Mwanga na Moshi vijijini. Zifuatazo ni baadhi ya picha ambazo zinaonesha uzuri wa Mkoa huu wa Kilimanjaro. Karibu
  
Nikiwa barabara ya Macheme nlifanikiwa kuupiga picha mlima   
     

 Wakati naelekea Rombo nilikuta ujenzi wa barabara unaendelea.

Moshi pazuri jamani, rangi ya kijani imetawala.

Menu ya Rombo kwa bibi

   Jana nilienda Rombo, nikapita kwa bibi. Ukaribisho wa kwanza ulikua ni mbege then hadithi za zamani kidogo. Halafu ikaja menyu, si unajua ndizi ndio menyu yetu ya maana.
 
 
Parachichi haliwezi sahaulika wakati wa ulaji wa ndizi, na hiyo ndio menyu yangu ya jana mchana, Shukrani kwa bibi.

Tuesday, May 3

Wali na Machalari- Lunch ya leo

Mchana wa leo nilikua na hamu ya kula chakula cha nyumbani. Nkawaomba wenyeji wangu wanipeleke ntakapopata hicho chakula. Moshi mjini karibu na TRA na Tanesco kuna sehemu yaitwa "Kwa Sigi". Hapo unapata menyu kadhaa za ukweli. Kuanzia ugali, mlenda, machalari, wali, samaki watoto a.k.a dagaa wote unapata hapo. Ukitembelea Moshi usiache kupitia hapo aiseeee.



Niliagizia wali na ndizi nyama, ni tamuuuu muno muno. Nkashushia na glasi ya mtindi freshhhh toka kwa ng'ombe.

Monday, May 2

Msaranga Special ya Golden shower - Moshi.

Mchana wa leo nimepelekwa na wenyeji wangu sehemu inaitwa Golden Shower. Niliambiwa kuna lunch special inatayarishwa yaitwa Msaranga Special. Binafsi niliagiza na viazi vya kuponda, Rogertus aliagiza na wali na Mkabita yeye aliagiza Fillet steak na chipsi.
Tulipofika wapishi ndo wakaingia kazini, nikapata bahati ya kufundishwa namna ya kupika hiyo Masaranga Special na Fillet steak. Naamini wali, viazi vya kuponda na chipsi tunajua kuvipika.
Naomba kushare na wewe mafundisho niliyoyapata..... Karibu.

Mahitaji:
  • Robo kilo ya fillet steak
  • Vitunguu swaumu (utavisaga)
  • Tangawizi (utaisaga)
  • Chumvi
  • Soya sauce
  • Vinegar
  • Kilo moja ya mdudu a.k.a pork (kata vipande vya wastan)
  • Pilipili hoho 1 (katakata vipande vidogo vidogo)
  • Royco curry powder
  • Nyanya 2 (zikwaruze / pondaponda)
  • Giligilani a.k.a korienda
Hatua za kupika:
Tuanze na fillet steak
  • Kwanza inapaswa kuimarinate nyama (kuiongeza ulaini na ladha), na hii inafanyika kwa kuchanganya vinegar, mafuta ya kupikia kidogo, soya sauce kidogo, tangawizi, kitunguu swaumu na chumvi kidogo kisha unaipaka nyama na kuiacha ikolee kwa muda 
  • Chukua kikaangio na uweke jikoni, ongeza mafuta ya kula na yapashe moto kwa muda
  • Kikaango na mafuta vikishapata moto, epua na uweke pembeni
  • Weka nyama iliyokua marinated kwenye kikaango, kisha kirejeshe kwenye moto
  •  
  • Wacha nyama iive kwa dk tano kisha igeuze iive upande wa pili kwa dakika 5 pia
  • Epua nyama yako tayari kwa kuliwa
Twende kwenye namna ya kupika hiyo Msaranga Special
  • Kwanza chemsha mdudu a.k.a pork pekee mpaka aive
  • Weka kikaango kwenye moto
  • Kisha ongeza mafuta, chumvi, vitunguu maji na pilipili hoho
  • Ongeza Royco mchuzi mix na koroga vichanganyike haswa
  •  
     
     
  • Ongeza nyanya ndani ya mchanganyiko huo ili upate ile rosti
  • Weka chumvi kiasi
  • Ongeza nyama ile tuliyochemsha, kisha weka soya souce kidogo
  • Ongeza maji uliyochemshia pork pale unapoona inakaukia
  •  
     
     
  • Weka giligilani a.k.a korienda
  • Tayari mlo upo tayari kwa kuliwa

  • Ukiweka mboga yako tayari na chakula cha kulia, ndo itatokea hivi:


Kama umependa mapishi, karibu upike na nitumie picha tuipate kushare na wenzetu
Asanteni Golden Shower

Sunday, May 1

Macaroni na Nyama ya kusaga

       Jumamosi ya tarehe 30.04.2011 Rafiqs zangu waliniambia wanapita kutoka ofisini wanaenda kwenye shughuli zao. Mida watakayopita ni ile mida ya Lunch, ikabidi nijipange. Nkaamua leo naingia jikoni mwenyewe. Tafutatafuta cha kupika, nkakutana na pakiti la macaroni kabatini na nyama ya kusaga kwa  jokofu. Nkakumbuka niliwahi fundishwa na mama yangu pishi hili. 
Karibu....Ukilipenda jaribu, halafu nitumie picha ya menu (chakula) itakavyotokea !!

Mahitaji:
  • Pakiti la macaroni  1            
  • Pilipili manga (utaisaga)
  • Chumvi
  • Blue band / Tanbond
  • Nyama ya kusaga
  • Kitunguu maji kikubwa 1 (kikate vipande vidogo vidogo)
  • Vitunguu swaumu (utaviponda)
  • Tangawizi (utaiponda)
  • Viazi ulaya (vikate vipande vidogo vidogo)
  • Biringanya (ikate vipande vidogo vidogo)
  • Pilipili hoho (ikate vipande vidogo vidogo)
  • Pilipili kali (iache nzima)
  • Karoti (ikate vipande vidogo vidogo)
  • Nyanya 2 (zikate vipande vidogo vidogo)
  • Tui la nazi (binafsi napenda lile la kukuna na kukamua mwenyewe)
  •               


Hatua za kupika:
Tuanze na Macaroni
  • Tayarisha sufuria safi, weka maji ya kutosha
  • Ongeza chumvi kiasi na pilipili manga iliyosagwa
  • Weka jikoni na yaache mpaka yachemke
  •                   
  • Ingiza macaroni kwenye maji yaliyochemka.
  • Japokua pakiti nyingi zinaandika kuwa muda wa kupika ni dakika 9 - 10, mi nashauri uhakikishe uivaji kwa kuzionja (unaweza kulisha watu kibichi)

  • Baada ya kuiva epua sufuria
  • Tayarisha chujio na mimina macaroni ndani ya chujio ili kuchuja maji uliyochemshia macaroni
  • Chukua maji yasiyo moto wala baridi miminia juu ya macaroni yakiwa bado ndani ya chujio
     
  • Rejesha sufuria uliyochemshia macaroni kwenye jiko huku ukiwa umepunguza sana moto
  • Weka Blueband/ Tanbond ndani ya sufuria yako na iacha iyeyuke vyema 
  • Rejesha macaroni ndani ya sufuria yenye Blueband/ Tanbond
  • Waweza ongeza pilipili manga iliyosagwa kama ukipenda
  • Koroga vyema kwa dakika 2 ili mchanganyiko wa macaroni, pilipili manga na Blueband/ Tanbond ukolee vyema 
  • Macaroni yako yapo tayari kwa kuchanganywa na mboga.
  • Epua sufuria weka pembeni na zima jiko


Tumalizie na Nyama ya kusaga:
  • Tayarisha sufuria safi, weka nyama ya kusaga peke yake bila ya kuweka maji
  • Ongeza chumvi kiasi, tangawizi na kitunguu swaumu
  • Weka sufuria lenye huo mchanganyiko kwenye jiko na washa jiko
  • Ongeza maji moto safi kila mara pale nyama inapokaukia
  • Funikia sufuria ili nyama ipate kuiva taratibu, hakikisha nyama imeiva vyema (ionje kama imeiva)
  • Baada ya kuiva epua nyama iweke kwenye chombo kingine pembeni.

  • Rudisha sufuria jikoni na weka mafuta ya kupikia kama vijiko vitatu
  • Ongeza chumvi kidogo, kisha weka vitunguu maji. koroga mchanganyiko huo (lazma utasikia harufu nzuri ya vitunguu vinaiva)
  • Vitunguu vikishaiva na kubadilika rangi ongeza pilipili kali moja bila kuikata
  • Ongeza vipande vya viazi na karoti na koroga
  • Ongeza biringanya, pilipili hoho na mchuzi ambao utakua upo katika ile nyama tuliyochemsha
  • Ongeza viungo kama vile vya pilau n.k (hapa inategemea unapenda viungo vipi, maana vipo vingi)

  • Vikishaiva ongeza nyanya, na ukorege kiasi kisha acha vichemke kidogo ili kutengeneza rojo
  • Weka nyama ya kusaga koroga vizuri huo mchanganyiko kisha acha kidogo vikolee
  • Waweza weka Royco mchuzi mix kama utapenda (mimi niliweka) kisha korogo rosti hilo
  • Malizia na tui na hakikisha unakoroga tui lisije kata
  • Baada ya tui kuiva vyema epua mboga yako tayari kwa kuchanganya na macaroni na kuliwa

  • Chukua chombo kingine tofauti, kikavu na kisafi (hotpot inafaa sana)
  • Weka macaroni yako kidogo, kisha unaweka mboga ya nyama ya kusaga kidogo kidogo huku unakoroga
  • Hakikisha macaroni na nyama vinachanganyika vyema.
  • Pakua chakula chako tayari kwa kuliwa.


Kama una swali, au maoni karibu sana sana!!!
Kama una mapishi yako unataka kutuletea karibu sana sana!!



Lunch ya Moshi

Lunch ya leo nimeagiza Cream of chicken kama kianzio, halafu msosi wenyewe ni Chicken curry na garlic naan. (Ntamtafuta mpishi anijuze utengenezaji wa hizi naan au chapati za kihindi).
 
 
Coke bariidi kwa pembeni ndo nashushia.  Shukrani kwa Impala hotel - Moshi kwa msosi huu. Karibuni Rafiqs!!!
Rafiqs, nasafiri kwenda Moshi. Naamini kuna vyakula mbalimbali ntaviona, ntavionja na kushare nanyi. Karibuni sana Moshi.
Kuna msemo, "Mcheza kwao hutunzwa". Naenda kutunzwa kwetu....... Aikambe/ Aikamai