Monday, July 30

Mapishi ya maandazi

   Wiki iliyopita katika moja ya pita pita zangu majumbani kwa watu, (maana mie nami mida mingine bila hata kukaribishwa huwa natokea tu milangoni mwa watu, na kwa sababu wananijua ni mmoja wa wana Menutime basi inakua rahisi kukaribishwa.) nikakatiza mitaa ya gerezani kule zamani kulikua na klabu ya Railway, ilijulikana kama Gerezani Railway Club, wazee wa zamani wanapafahamu maana ndo walikua wanajidai kama vijana wa kisasa wanavyojidai Maisha Club na kadhalika. Basi nyumbani kwa mama Mzuka nikakaribishwa maandazi, nikala, nikafunga mengine ili namie wanafamilia wangu wajaribu kidogo.
  Siku inayofuata ikabidi nitafute namna ya kwenda kuomba kufundishwa namna ya kupika maandazi. Nikapangiwa muda na juzi ndo nilifundishwa namna ya kupika. Karibuni marafiq wa MenuTime tujifunze wote namna ya kupika maandazi.

Mahitaji:
  • Unga wa ngano - kilo 1
  • Hamira - vijiko 4 vidogo
  • Sukari - vijiko 7
  • Blue band  - vijiko 7
  • Tui la nazi  - nazi nzima moja (kwenye kutengeneza tui tenga la kwanza na la pili)
                        
Hatua:
  • Chukua chombo kikavu, kama ni sufuria au kijibeseni kidogo kama cha mama Mzuka hapo juu. Weka unga wako, ongeza blueband, sukari, hamira na changanya vyema mchanganyiko wako. (Iwapo utapenda maandazi yako yawe na iliki, huu ndo muda wa kuziweka iliki zako zikiwa zimetwangwa)
  • Ongeza tui la kwanza kwenye ule mchanganyiko wa unga wa ngano na vinginevyo, kisha anza kuuchanganya kwa kutumia mikono. Changanya vyema kisha anza kuukanda unga wako ukiwa na mchanganyiko wa mambo yote hayo juu
  • Ongeza tui mara kwa mara huku ukiendelea kuukanda unga wako, mpaka pale huisikii sukari mkononi (hapa kama naelewana na wenye mazoea ya kupika auuuuu, ni hivi kuisikia sukari mkononi ni wakati unakanda unavigusa vipunje vya sukari), sasa kanda mpaka unga uwe laini na huvisikii hivo vipunje mkononi... upo? tuendelee sasa
  • Viringisha mchanganyiko wako kwani upo tayari kwa hatua nyingine. Malizia kwa kuupaka blue band kwa juu kisha uache kwa muda wa takribani dakika 10 - 12 hivi, ili upate kuumuka vyema. Hapa hamira inafanya kazi yake sasa
  • Angalia jinsi unga wetu ulivyotokelezea (kama wasemavyo vijana wa kisasa)


  • Baada ya hapo tengeneza vipande vidogovidogo vya mviringo toka kwenye ule mviringo mkubwa     waweza toa kama vipande 8 - 10 wewe tu na mapenzi yako
  • Tazama mfano hapo chini



  • Kifuatacho ni kusukuma ule unga wako. Sasa kama unakibao cha kusukumia na fimbo yake vyema sana,(hii inaonesha jinsi gani jiko lako limekamilika), kama huna basi tumia njia mbadala ambayo ni safisha meza yako na kausha iwe kavu, kisha chukua chupa ya bia iliyo tupu, safisha na kausha tayari kwa kutumia kusukumia unga wako
  • Paka unga wa ngano kidogo sehemu ambayo utasukumia maandazi yako kama ni mezani au kwenye kibao (sie tulikua na kibao)
  • Kisha kata kipande kidogo cha kujaa mkono kutoka katika moja ya vile vipande vyako 8 - 10, kisha anza kukisukuma kwenda mbele na nyuma ili kuweza tengeneza umbo la duara
  • Endelea kusukuma mpaka unaona unga unakua kama shepu ya chapati ila angalia isiwe nyembamba sanaaa au nene sanaa. Yaani iwe saizi ya kati kama uionavyo hapo kwenye picha chini



  • Sasa maandazi yako yapo tayari kukatwa katika shepu tofautitofauti kutokana na mapenzi yako.
  • Angalia hapo chini sie tulivyoamua dizaini mbalimbali
  • Hii ilitoa maandazi ya mraba



  • Hii ilitoa yale maandazi madogo madogo ya kijimviringo



  • Mama akaniambia hata glass yatumika katika kuweka shepu ya mviringo



  • Afu mwisho akasema tunaweza kusuka maandazi, nikaamini ubunifu upo pande zote na kwa mama mmmmh kuna mengi ya kujifunza



  • Utani utani tukajaza nyungo tatu na dizaini mbalimbali za maandazi  ambayo yapo tayari kwa hatua ya mwisho



  • Sasa yaache maandazi kama kwa muda kama dakika 5 hivi ili hamira imalizie kufanya kazi yake, na muda huo weka mafuta kwenye kikaango kisha weka motoni ili yapate moto



  • Anza kuchoma maandazi yako kwa kuyaweka kwenye kikango chenye mafuta yalochemka.
  • Weka kwa kiasi na yasibanane sana, angalia hapo chini yanavyowekwa kwa nafasi



  • Baada ya dakika kadhaa yachungulie kama yameshaanza kubadilika rangi na kuwa ya brown a.k.a rangi ya udongo, kisha yageuze upande wa pili ili yapate kuiva pia



  • Yataonekana kama hivibaada ya kugeuzwa



  • Epua maandazi yako kwani yapo tayari kwa kuliwa.


  •    Mwisho wa shughuli utakua na picha kama hii hapa chini. Waweza kuyala maandazi yako muda wowote na wayala peke yake maana ni laini, au ukamezea na maji safi ya kunywa. Ukipenda na juisi fresh na maziwa na soda yaani ni wewe tu na kimiminika ukipendacho.

       Tulipata request nyingi za kutaka kujifunza namna ya kupika maandazi na kama tunavyoahidi, tunatimiza ahadi zetu, nia yetu ni kufundishana namna ya kupika vyakula mbalimbali, kujuzana sehemu za kupata mlo na mengine mengi yahusuyo chakula na ndo maana tukaitwa MenuTime.
       Shukrani za dhati sana kwa mama Peter Mzuka, kutukubalia kutufundisha ili tuweze kuwafundisha wengine. Asante sana.
       Tujuze wataka kujifunza kipi kingine, tuoneshe picha baada ya kujaribisha kupika upishi huu kwa kupitia anwani yetu menutimes@gmail.com au menutimetz@gmail,com nasi tutashare na wenzetu pande zote duniani.
       Kutoka gerezani LJM nawafundisha.

    14 comments:

    1. nitajaribu yenye iliki, nijue yatatokeaje

      ReplyDelete
    2. Asanteni sana kwa kutufundisha mapishi, naomba wiki hii mtufundishe jinsi ya kupika Chapati.

      ReplyDelete
    3. Thanks alot kwa mafunzo ya mapishi ila naomba mnaposema vikombe 2 au 3 mtuoneshe vya saizi gani tusije pimia majagi jamani.






      ReplyDelete
    4. Mandazi matamu hayoooooooooooooooo!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!! Hongera sana

      ReplyDelete
    5. Tunashukuru sana kwa kutufumbua macho!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!

      ReplyDelete
    6. Mashallah, tunashkuru kwa mapishi.ok acha nitengeneze sasa mh! Kwa blueband/sunflower margarine

      ReplyDelete
    7. Tunashukuru kwa maoni yenu Rafiqs wote hapo juu.
      Mama Hajj, wakati tunakanda tulifundishwa tutumie blueband, na tukaonesha ni vijiko saba vya blue band vitahitajika. Wakati wa kukaanga sasa, waweza tumia mafuta ya maji aina yoyote uipendayo, maana tunapishana kwenye mapenzi ya utumuaji wa mafuta ya kula. Kuna wanaopenda sunflower, korie nakadhalika, haijalishi sana aina inategemea na wewe na mapenzi yako tu katika ukaangaji. Naamini tumekujibu vyema, na endelea kututembelea, pia tupo katika mitandao ya jamii kama twitter, instagram na tuna page yetu katika facebook. Karibu sana na uwe na Ijumaa njema

      ReplyDelete
    8. Jane tutafanyia kazi maoni yako kuhusu kipimo cha kikombe

      ReplyDelete
    9. Rafiq tutafanyia kazi maoni yako, na tutarejea kuwafundisha namna ya kupika chapati

      ReplyDelete
    10. Ahsante sana mpendwa kwa maelezo yako yakinifu...nimekupata vema!

      ReplyDelete
    11. Asanteeee sana mpendwa naenda kuiaribu sasahv ,,,,,

      ReplyDelete
    12. Asante kwa mapishi ya mandazi

      ReplyDelete