Jumapili ya jana nikasema kwanini nisipike keki toka mwanzo, maana nimezoea kununua ule unga uliyotayarishwa kisha nafanya kuongeza mayai, maziwa kisha naweka mchanganyiko kwenye kikaangio cha kuokea keki tayari kwa kuoka. Ila leo nkaona nianze toka mwanzo hadi mwisho.
Jiunge nami hatua kwa hatua
Mahitaji:
- Unga wa ngano - vikombe viwili na nusu
- Siagi - kikombe kimoja
- Sukari nyeupe - Kikombe kimoja na robo tatu
- Mayai - 3
- Vanilla extra - kijiko cha chai kimoja na nusu
- Maziwa - kikombe kimoja na nusu
- Unga wa Cocoa usio na utamu sana (Unsweetened Cocoa powder) - vijiko vya mezani 6
- Baking soda - kijiko cha chai kimoja na nusu
- Chumvi - kijiko kimoja
Hatua:
- Washa jiko la oveni katika nyuzi joto 350. Pakaa siagi kwenye kikaangio, kisha nyunyuzia unga kidogo. Changanya unga, Cocoa, baking soda na chumvi pamoja, kisha weka pembeni.
- Katika bakuli kubwa, changanya siagi na sukari, koroga mchanganyiko huo mpaka uwe laini sana, ongeza mayai, moja baada ya lingine kwa awamu huku unakoroga vyema mchanganyiko huo, kisha ongeza vanilla, changanya vyema mchanganyiko huo.
- Katika bakuli kubwa lenye mchanganyiko wa siagi, sukari,mayai na vanilla ongeza kwa kupishana mchanganyiko wa unga na maziwa huku unakoroga vyema. Endelea kufanya hivyo mpaka unga na maziwa vyote viishe na kuchanganyika vyema na mchanganyiko wa siagi.
- Oka keki katika oven uliyoiwasha mapema kwa muda wa dakika 40 mpaka 45, kuhakikisha kama imeiva vyema tumbukiza kijiti kisafi cha mbao au toothpick katikati ya keki na kuchomoa. Iwapo itatoka yenyewe ikiwa safi bila chenga chenga basi ujue keki yako imeiva.
Keki yako ipo tayari kwa kuliwa, waweza kuila na kinywaji kama soda, juisi, maziwa au hata chai, wewe tu na uchaguzi wako.
Kama umeipenda basi jaribisha na wewe kupika, na kama una namna ingine ya kupika keki ya chokolate tafadhali tujuze nasi kupitia anuani hii menutimes@gmail.com.