Tuesday, July 31

Menyu toka Newburry - Great Britain a.k.a UK

   Ni raha pale ambapo tunajuzwa marafiq wanakula nini pale walipo. All the way kutoka Newburry - Great Britain a.k.a UK na sio Ukonga, rafiq yetu Hellen ametujuza kile alikua anakula jana kwa kupitia email zetu.
   Kwenye sahani yake hapo chini kuna mkate uliookwa a.k.a toasted bread, baked beans, sausages na bacons.

   Glass inachungulia hapo kulia pembeni hakika ilitumika katika kuweka kimiminika mbacho bidada alikua anakitumia wakati wa kupata mlo wake
   Da Hellen Asante sana kwa kutujuza na kushare nasi.





Monday, July 30

Mapishi ya maandazi

   Wiki iliyopita katika moja ya pita pita zangu majumbani kwa watu, (maana mie nami mida mingine bila hata kukaribishwa huwa natokea tu milangoni mwa watu, na kwa sababu wananijua ni mmoja wa wana Menutime basi inakua rahisi kukaribishwa.) nikakatiza mitaa ya gerezani kule zamani kulikua na klabu ya Railway, ilijulikana kama Gerezani Railway Club, wazee wa zamani wanapafahamu maana ndo walikua wanajidai kama vijana wa kisasa wanavyojidai Maisha Club na kadhalika. Basi nyumbani kwa mama Mzuka nikakaribishwa maandazi, nikala, nikafunga mengine ili namie wanafamilia wangu wajaribu kidogo.
  Siku inayofuata ikabidi nitafute namna ya kwenda kuomba kufundishwa namna ya kupika maandazi. Nikapangiwa muda na juzi ndo nilifundishwa namna ya kupika. Karibuni marafiq wa MenuTime tujifunze wote namna ya kupika maandazi.

Mahitaji:
  • Unga wa ngano - kilo 1
  • Hamira - vijiko 4 vidogo
  • Sukari - vijiko 7
  • Blue band  - vijiko 7
  • Tui la nazi  - nazi nzima moja (kwenye kutengeneza tui tenga la kwanza na la pili)
                        
Hatua:
  • Chukua chombo kikavu, kama ni sufuria au kijibeseni kidogo kama cha mama Mzuka hapo juu. Weka unga wako, ongeza blueband, sukari, hamira na changanya vyema mchanganyiko wako. (Iwapo utapenda maandazi yako yawe na iliki, huu ndo muda wa kuziweka iliki zako zikiwa zimetwangwa)
  • Ongeza tui la kwanza kwenye ule mchanganyiko wa unga wa ngano na vinginevyo, kisha anza kuuchanganya kwa kutumia mikono. Changanya vyema kisha anza kuukanda unga wako ukiwa na mchanganyiko wa mambo yote hayo juu
  • Ongeza tui mara kwa mara huku ukiendelea kuukanda unga wako, mpaka pale huisikii sukari mkononi (hapa kama naelewana na wenye mazoea ya kupika auuuuu, ni hivi kuisikia sukari mkononi ni wakati unakanda unavigusa vipunje vya sukari), sasa kanda mpaka unga uwe laini na huvisikii hivo vipunje mkononi... upo? tuendelee sasa
  • Viringisha mchanganyiko wako kwani upo tayari kwa hatua nyingine. Malizia kwa kuupaka blue band kwa juu kisha uache kwa muda wa takribani dakika 10 - 12 hivi, ili upate kuumuka vyema. Hapa hamira inafanya kazi yake sasa
  • Angalia jinsi unga wetu ulivyotokelezea (kama wasemavyo vijana wa kisasa)


  • Baada ya hapo tengeneza vipande vidogovidogo vya mviringo toka kwenye ule mviringo mkubwa     waweza toa kama vipande 8 - 10 wewe tu na mapenzi yako
  • Tazama mfano hapo chini



  • Kifuatacho ni kusukuma ule unga wako. Sasa kama unakibao cha kusukumia na fimbo yake vyema sana,(hii inaonesha jinsi gani jiko lako limekamilika), kama huna basi tumia njia mbadala ambayo ni safisha meza yako na kausha iwe kavu, kisha chukua chupa ya bia iliyo tupu, safisha na kausha tayari kwa kutumia kusukumia unga wako
  • Paka unga wa ngano kidogo sehemu ambayo utasukumia maandazi yako kama ni mezani au kwenye kibao (sie tulikua na kibao)
  • Kisha kata kipande kidogo cha kujaa mkono kutoka katika moja ya vile vipande vyako 8 - 10, kisha anza kukisukuma kwenda mbele na nyuma ili kuweza tengeneza umbo la duara
  • Endelea kusukuma mpaka unaona unga unakua kama shepu ya chapati ila angalia isiwe nyembamba sanaaa au nene sanaa. Yaani iwe saizi ya kati kama uionavyo hapo kwenye picha chini



  • Sasa maandazi yako yapo tayari kukatwa katika shepu tofautitofauti kutokana na mapenzi yako.
  • Angalia hapo chini sie tulivyoamua dizaini mbalimbali
  • Hii ilitoa maandazi ya mraba



  • Hii ilitoa yale maandazi madogo madogo ya kijimviringo



  • Mama akaniambia hata glass yatumika katika kuweka shepu ya mviringo



  • Afu mwisho akasema tunaweza kusuka maandazi, nikaamini ubunifu upo pande zote na kwa mama mmmmh kuna mengi ya kujifunza



  • Utani utani tukajaza nyungo tatu na dizaini mbalimbali za maandazi  ambayo yapo tayari kwa hatua ya mwisho



  • Sasa yaache maandazi kama kwa muda kama dakika 5 hivi ili hamira imalizie kufanya kazi yake, na muda huo weka mafuta kwenye kikaango kisha weka motoni ili yapate moto



  • Anza kuchoma maandazi yako kwa kuyaweka kwenye kikango chenye mafuta yalochemka.
  • Weka kwa kiasi na yasibanane sana, angalia hapo chini yanavyowekwa kwa nafasi



  • Baada ya dakika kadhaa yachungulie kama yameshaanza kubadilika rangi na kuwa ya brown a.k.a rangi ya udongo, kisha yageuze upande wa pili ili yapate kuiva pia



  • Yataonekana kama hivibaada ya kugeuzwa



  • Epua maandazi yako kwani yapo tayari kwa kuliwa.


  •    Mwisho wa shughuli utakua na picha kama hii hapa chini. Waweza kuyala maandazi yako muda wowote na wayala peke yake maana ni laini, au ukamezea na maji safi ya kunywa. Ukipenda na juisi fresh na maziwa na soda yaani ni wewe tu na kimiminika ukipendacho.

       Tulipata request nyingi za kutaka kujifunza namna ya kupika maandazi na kama tunavyoahidi, tunatimiza ahadi zetu, nia yetu ni kufundishana namna ya kupika vyakula mbalimbali, kujuzana sehemu za kupata mlo na mengine mengi yahusuyo chakula na ndo maana tukaitwa MenuTime.
       Shukrani za dhati sana kwa mama Peter Mzuka, kutukubalia kutufundisha ili tuweze kuwafundisha wengine. Asante sana.
       Tujuze wataka kujifunza kipi kingine, tuoneshe picha baada ya kujaribisha kupika upishi huu kwa kupitia anwani yetu menutimes@gmail.com au menutimetz@gmail,com nasi tutashare na wenzetu pande zote duniani.
       Kutoka gerezani LJM nawafundisha.

    Saturday, July 28

    Menyu kutoka Entebe - Uganda

       Menu Time tupo Dar iliyo salama, Tanzania. Lakiniiii tuna marafiq sehemu mbalimbali yaani kila kona ya dunia. Na marafiq hawa hupenda kushare nasi vitu vitamu ambavyo wanakula.
       Kutoka Entebe Uganda, Mashariki ya Afrika tumeletewa  picha hii na Rafiq yetu, ambaye wazazi wake wamempa jina la Baraka Ntanga.
       Ni samaki aina ya sato na vipande vya viazi a.k.a chipsi. Kalimau hako katakua ndo kikorombwezo chake Baraka.

       Tutumie na wewe kutoka popote ulipo picha ya menyu yako kupitia email address zetu menutimes@gmail.com au menutimetz@gmail.com nasi tutashare n a wengine. Karibuni sana!!
       Kutoka uganda, tunasema Webale sebo Baraka

    Thursday, July 26

    Mikate Mikate Mikate

       Mara nyingi tumezoea kula mkate uliopikwa kwa kutumia unga wa ngano. Nimeamini binadamu ni watundu mno, au niseme wabunifu???..... naamini neno wabunifu litafaa zaidi. Wahenga walisema "tembea uone"... na sie leo tumejionea.
      Kutoka kwa Rafiqs zetu, Menu Time tumejuzwa maeneo ya kupata aina tofauti ya upikwaji wa mikate, nasi tukaona ni vyema kuwajuza. Najua wengi mtasema mbona mpiko huu wa mkate tunaujua..... si ndio? sawaaa wa kwanza ntakubali ila huu mwingine naamini ndo sie tutakua tunawajuza wengi wenu.
     Tunaongelea mkate wa kumimina, kama uonekanavyo kwenye picha hapo chini... huu unapatikana mitaa ya upanga uhindini kama wanavyopaita wenyewe.
                               

       Huu wa pili ni mkate wa tambi, yaani umetengenezwa kwa tambi. Sasa ni namna gani umetengenezwa bado hatujapata ubunifu wake, ila hivi karibuni vyote vikienda sawa tutawajuza, laaa tutawajulisha wapi unapatikana nawe uweze kuuonja.
     

        Mikate hii hupatikana kwa kutoa oda, yaani upige simu siku moja kabla ili waweze kukutengenezea maarn utamu wake ni kwamba uliwe siku hiyo hiyo au walau keshoye asubuhi yaani uchukuliwe jioni uliwe asubuhi lakini usiuweke ukae saaana, unakua kama umepoa hivi. 
                               
    Shukrani za dhati ziwafikie Janeth, Peter na da Bridget kwa kutuonesha na kutuelekeza wapi twaweza kupata utamu huu.
      Kutoka pande za upanga, MenuTime yawajuza.

    Mokka City Cafe & Lounge ya City center mjini Dar iliyo salama

       Mjini Dar iliyo salama, naongelea katikati ya mjini haswaa, yaani pale Samora ambapo mambo yote unayapata kuanzia fundi wa saa, hadi wa simu. Yaani wenye mji wenyewe wanasema kila kitu hupatikana hata mihuri ya naniihii (jina limenitoka kidogo) inapatikana hapo, ndipo huu mgahawa ulipo. Unaitwa Mokka City Cafe & Lounge na hauna muda mrefu saana toka umefunguliwa, naongelea sio zaidi ya miezi mitatu hivi.
       Humo ndani kuna mengi muno muno, ila leo ngoja tuongelee machache ili nawe upate hamu ya kwenda kupatembelea hivi karibuni.
       Menu Time tutaongelea vimiminika tu siku ya leo... na tunaanza na hiki.
    Tuliambiwa kinaitwa Ice Mocha na hivyo vipande unaona ni vya barafu. Sasa kinatengenezwaje ni siri yao ila MT tunadhibitisha utamu wake kwani baadhi ya wanachama wa MT walipata kukionja.
     
     
       Mara ya kwanza sisi kufika hapa tulilakiwa na harufu nzuri ya kahawa, yaani ukiingia tu ndani ya mlango unaachia tabasamu uwe mpenzi au sio mpenzi wa kahawa, ila harufu yake laaaaah, lazima uagizie kinywaji chochote kilichotengenezwa na kahawa.
    Ya pili wanaiita Cappuccino

       Kila mmoja wetu ana mbwembwe zake katika idara yake. Kinyozi ajua kunyoa vyema na kuchonga style, msusi atakusuka nywele utadhani mkeka, basi na watengenezaji kahawa wa Mokka city nao wana mbwembwe zao katika kurembesha hiyo Cappuccino yao.
      Moja ya mbwembwe zao ni hii ambayo imerembwa mfano wa jani hapo juu.... nimependa ujuzi huu
     
       Wakati tunaendelea kushangaa urembo na mandhari, manager wa Mokka City aitwa  Ben akasema hiyo mbona cha mtoto,  kisha akatuletea Cappuccino ingine yenye urembo mfano wa nyumba ya buibui.
       Tazama usanii, ubunifu na kazi iliyofanyika hapo.

          Ukiwa mjini na unahitaji sehemu ya kupumzika , kupata kikombe cha kahawa, chai, iwe juisi, maji baridi hata soda, chakula na vinginevyo usisite kufika Mokka City Cafe & Lounge ambayo ipo barabara ya Samora, mkabala na jengo la IPS.
        Kutoka Mokka City Cafe & Lounge, LJM wa Menu Time nawapasha.

    Wednesday, July 25

    Menyu kutoka Zuane Trattoria Pizzeria iliyopo Oyster bay - DSM

       Popote mlo wapatikana, kubadilisha mandhari ndio mpango mzima. Tumerejea Dar iliyo salama baada ya mapumziko na haya ndiyo yaliyojiri......
       Hii sehemu naongelea Zuane Trattoria Pizzeria inahusika sana na menyu zenye asili ya uitaliano, ni muhimu kupatembelea ili nawe upate ladha tofauti kidogo. Sio lazma tusafiri kwenda Italy tuweze onja ladha ya menyu zao laaaah, wamekusogezea hadi mlangoni hapa Dar iliyo salama.... kazi kwako.
    Ya kwanza naileta kwenu yaitwa Lasagne, ndo hii hapa
    Ya pili ni tambi na sea food haswaa yafahamika kama "Spaghetti ai fruttidi mare" Naamini jina lipo sawa!!!.

    Tutarejea kuwajuza mengineyo mengi kutoka pande za uzunguni kama inavyojulikana, naongelea Oysterbay
    Toka Zuane LJM wa Menu Time naarifu.

    Tuesday, July 24

    Halwa

    Halwa ni moja ya vyakula vinavolika sana wakati wa mfungo wa Ramadhan, Basi Mdau mmoja Wa MT aitwa Adilu alitukaribisha Halwa na sie bila hiyana tukaone tushiriki nanyi katika mwezi huu.. inshaalah basi jongea maduka ya tende na Halwa nawe upate Yakheeeee..!
    Basi unamega kipande cha kadri yako alafu unafurahia utamu wa halwa


    Menyu toka Bagamoyo

      Baada ya purukushani za mjini Dar iiyo salama, wanafamilia waliamua kwenda nje kidogo ya mji kwenda kupunga upepo na kubadilishana mawazo. (Ni jambo jema kufanya mara upatapo mda, na inashauriwa hivyo, kwani hufanya akili kupumzika na kuweza fikiria vyema katika kupanga mipango yako ijayo)
      Kama ilivyo ada huwezi enda sehemu ikapita bila kupata menyu, na yafuatayo ndiyo yaliyojiri.
    Viazi a.k.a chipsi, salad na kuku masala.
    

       Pia kulikua na viazi vya kuponda a.k.a mashed potatoes, na salad pamoja na kuku inayoitwa Chachandu chiken katika menyu ya Livingstone Beach Resort


    Nyumbani ni nyumbani kuna walioamua kupata huyooo chachandu chiken pamoja na ugali.

       Cha ajabu kilichokutwa katika menu ya resort ya Livingstone beach ni ukosefu wa sea food na red meat, naongelea nyama ya n g'ombe, na nyinginezo. hivyo iliwapasa wanafamilia hao kuagizia kilichopo ambacho ni kuku.
       Ukipata kwenda nje ya mji, kupata kupunga hewa tujuze kupitia menutimes@gmail.com
    Kutoka Bagamoyo, LJM naarifu.

    Monday, July 23

    Kikorombwezo

      Baada ya kuzungumzia vikorombwezo, wengine mekutana nao ambao kikorombwezo chao ni mchanganyiko wa pilipili kichaa na vinegar pamoja na chumvi.Ila niliambiwa badala ya vinegar pia waweza tumia ndimu au limau, mapenzi yako tu wewe na kikorombwezo chako.
      Pata uone muonekano wa Rafiq wa Menu Time a.k.a MT

    Tujuze kikorombwezo chako kupitia menutimes@gmail.com nasi tutashare na wenzetu humu ndani.

    Sunday, July 22

    Chungu Cha Pili.

    Hapa Matumbo ya waumini wengi hayajazoea kula chakula kingi kwa wakati mmoja, hivo chungu cha pili bado kina mlo kidogo ukilinganisha na chungu cha kwanza......... chungu chetu leo kina viazi ulaya, njugu mawe, mihogo, samaki chapati na Uji.
    Karibu sana

    Saturday, July 21

    Chungu Cha Kwanza.

    Unapokuwa unafuturu katika mwezi wa Ramadhani sio lazima uwe na kundi kubwa la chakula, Jaribu kufuturu kulingana na mfuko wako na chakula utakachoweza kumaliza. Hii ni Futari Ambayo waweza kula kama Bachelor.

    Nyama ya Kukaanga, yai la kukaanga na embe.... ongeza na maziwa fresh ya moto.

    Futari kwa niaba ya watu wa Menu Time. Ramadhan Karim.

    Friday, July 20

    Korosho Toka Kwa Dada Christina.

    MT inao marafiki wengi kutoka pande mbalimbali Duniani, Christina a.k.a Mama Steve ni mmoja wa Marafiki wa MT, Basi katika Safari zake za Kikazi alitembelea Mkoa wa Mtwara.. wenyewe wanaita Ntwara. Mara akakutana na Korosho, Kutokana na mapenzi yake kwa MT kitu cha kwanza kufikiria ilikuwa ni kutununulia Korosho kutoka.. Ntwara zikapandishwa ndege.. zikafika JK Nyerere Int. Airport njia nzima na foleni za Dar, Mpaka zikafika Mikononi mwa MT. Tunajivunia kuwa na Rafiki kama Christina.

     Karibu Korosho za Ntwaraaaaa....

    Thursday, July 19

    Chachandu

      Kila mmoja wetu ana kikorombweza au niseme vikorombwezo ambavyo anapenda kusindikizia mlo wake. Kuna wanaopenda pilipili, tomato sauce, mayonnaise, chilli sauce na vinginevyo vingi tuu. Mjini Songea nilipotembelea nililetewa hii chachandu ambayo imejazwa pilipili za kutosha.
      Sio kimuonekano tuu, bali hata ladha yake ni tamu. yaani inawasha kwa sababu ya pilipili, halafu hutaki kuiacha kwasababu ya utamu. Hapo sasa!!!!


      Binafsi inategemea nakula chakula gani ndo niangalia nasindikiza na kikorombwezo gani. Tujuze wewe unapendelea kipi, na zaidi tutumie kwa picha nasi tujue, pengine tukijaribu na kukiienjoy. Karibuni sana!!

    Wednesday, July 18

    Tupike ndizi na Smoked beef

        Leo tuangalie ile nyama ya kupikwa kwa moshi a.k.a smoked beef inavyopikwa na ndizi kupitia mapishi ya kichagga. Upishi hili nimefundishwa na mama yangu mzazi. Mama Lulu.

      Hapa nilitumia nusu kilo ya smoked beef, ndizi mbili (ila kwenye upande wa aina ya ndizi, waweza chagua iwe mshale au bukoba yaani wewe na mapenzi yako).

      Kuniuliza inapatikana wapi hii nyama, ni Peramiho, mkoani Songea. Nilipopata bahati ya kutembelea mkoa wa Songea, Rafiq wetu aitwa Deo aliniagiza mzigo toka kwa mama mdogo. Mama mdogo alinipa zawadi ya kilo moja ya smoked beef.... nilishukuru saana. Za pekee shukrani zimwendee Deo kwa kutujuza kuhusu hii nyama tamu.

      Baasi tuanze kupika sasa,
    Tayarisha sufuria yako, kisha menya ndizi zako, katakata vipande, zioshe vyema, kisha ziongezee maji safi, chumvi kiasi. Ongeza vipande vyako vya smoked beef ndani ya sufuria hilo. Katakata kitunguu maji kimoja, pilipili hoho moja, nyanya mbili kisha changanya na zile ndizi. weka jikoni, funikia acha viive.

    Namna ya kugeuza mapishi haya ni kwa kuyapepeta, ndiooooo, shikilia sufuria lako na vitambaa kuepusha kuungua na kisha pepeta ili mchanganyiko wa juu ushuke chini na wa chini upande juu na viweze kuiva vyema. onja kama vimeiva na kama tayari basi zima jiko epua mlo wako tayari kwa kuliwa.
    Mimi wa kwangu ulionekana hivi.....
                               
     Jaribisha hii, ila Mama alisema waweza tumia nyama ya kawaida yaani isiyo smoked, na utapata utamu kama huo hapo juu au tofauti kidogo katika ladha.
     Tujuze ya kwako inatokeaje baada ya kujaribu kwa kututumia picha yako kupitia barua pepe: menutimes@gmail.com au menutimetz@gmail.com nasi tutashare na wengine.
    Kutoka jikoni kwa MenuTime LJM naaga.

    Monday, July 16

    Upishi wa Sato na Yai.

    Muda mwingine tukiamka asubuhi tunahitaji kifungua kinywa cha haraka ili tuwahi kazini.. Hii ni moja ya vifingua kinywa unavyoweza kuandaa kwa haraka zaidi.
    • Samaki (sato)
    • Nyanya na kitunguu
    • Mayai matatu



     Kaanga mayai kwanza, kisha yaweke pembeni.    
    •  Weka samaki wako kwenye sufuria na maji ya kutosha kisha injika kwenye moto
    • katakata nyanya na vitunguu kisha weka pamoja kwenye sufuria moja na samaki
    • Acha nyanya na samaki vichemke pamoja ila usiweke mafuta, bali tia chumvi kidogo

    Uache mlo wako uchemke mpaka rangi ibadilike na kuwa ya njano, Kisha weka yai lako na ufurahie mlo.

     karibuni sana

    Thursday, July 12

    Breakfast.

    Inashauriwa tunapoamka asubuhi tufungue kinywa kwa kitu chochote cha moto, Basi ile kuamka tu nikaamua nichemshe samaki (Sato) pamoja na Mayai ya kukaanga...
     wenyewe wanaiita Breakfast ya kukata na shoka.. ilikuwa tamu sana ijaribu sasa hivi......

    Sunday, July 8

    Ndizi Nyama.

    Ndizi nyama ni miongoni mwa vyakula asilia kabisa katika nchi ya Tanzania, Ndizi hupikwa kwa mitindo mbalimbali kama ambavyo MT imekuwa ikionesha mara kwa mara...http://menutime.blogspot.com/2012/01/matoke-ya-dada-megvicta.html
    Mapishi mbalimbali ya matoke yatakuijia kadri tutakavoyapata.. furahia chakula na Menu Time.

    Karanga, Popcorn na Visheti.

    Meno ya Binadamu yanapenda kutafuna tafuna mara zote.. wengine hutafuna Big G ili kuchangamsha meno na kinywa.. lakini pia Popcorn a.k.a Bisi, Visheti na Karanga ni miongoni mwa vichangamsha kinywa vizuuuuuri sana.
     Ukipata na visheti pia waweza kuvichanganya na Popcorn zako afu ukala kwa pamoja, ni tamu haswaaaaaaa
     waweza pia kuandaa karanga na kuchangamsha kinywa chako pia....
     Jiunge nasi kila siku kwa aina mbali mbali za Menu...