Kwenye familia naamini kuna baadhi ya ndugu ambao hupenda kupika ila hawapendi kukaa muda mwingi jikoni wakiwa wanapika, na kwa sababu hiyo huchagua kutengeneza ile miilo ambayo ni rahisi kutengeneza na haichukui muda mwingi uwepo wa mpishi jikoni.
Njia ni tofauti, yaweza kutumia njia ya kupika kwa moto mdogo mda mrefu, hivyo baada ya matayarisho mpishi yakupasa kurejea mara kwa mara jikoni kuangalia je, mapishi yanaendaje??
Leo tunawasaidia wale wa aina hiyo, yaani hutaki kukaa muda mwingi jikoni ila wataka kula chakula kizuri na kitamu. Tunapika samaki leo. Samaki ni wa aina ya Sato.
Mahitaji:
- Samaki sato 3
- Chumvi kiasi
- Pilipili manga kiasi
- Kitunguu swaumu 1
- Tangawizi 1
- Vinegar vijiko 2
- Ndimu 1
- Mafuta kiasi
- Pilipili hoho 1
- Karoti 1
- Nyanya 2
- Kitunguu maji 1
Hatua:
- Changanya mafuta kiasi, vinegar, ndimu, chumvi, pilipili manga, kitunguu swaumu, tangawizi (zilizopondwa)
- Katakata samaki vipande, yaani samaki mmoja akatwe mara tatu, kisha mchane kwa pembeni kiasi ili kuruhusu viungo viingie ndani ya minofu
- Paka samaki kwa mkono viungo ulivyochanganya juu kisha vichanganye vipande vya samaki kwa pamoja vipate kuchanganyika vyema
- Katakata pilipili hoho, karoti, nyanya na vitunguu maji katika vipande vikubwa kidogo
- Changanya samaki waliopakwa viungo pamoja na mchanganyiko wa vipande vya pilipili hoho , vitunguu maji na kadhalika (viache kwa nusu saa ili viungo viikolee vyema)
- Chukua tray kwa ajili ya kuweka kwenye oven, paka mafuta kiasi ili kuondosha kukaukiwa kwa samaki juu ya trey
- Weka mchanganyiko wote juu ya trey uliotayarisha, na itaonekana kama ilivyo kwenye picha hapo chini
- Moto wa oven utakaoanza nao ni 180
- Kwa karibu utaona kuna rojo limejitengeneza kutokana na viungo ulivyoweka. Linahitajika kusaidia samaki kuiva bila ya kuungua
- Baada ya dakika 20 hivi, trey yako itaonekana hivi, samaki wanaanza kuiva kwa taratiibu sana
- Baada ya dakika 45 toka kuweka samaki wako kwenye oven, punguza moto mpaka 130 kisha jipe dakika nyingine kama 10 hivi na uzime jiko kabisa na hapo samaki wako watakua tayari, kama waonekanavyo kwenye picha
- Waweza kula samaki hawa kama mboga na chakula chochote. Sisi tulikua na wali mweupe uliochanganywa na njegere, kulikua na maharagwe pamoja na mchicha uliokaangwa na vitunguu maji na karoti. Na sahani yetu ilionekana hivi..... pembeni ni vile vipande vya nyanya, vitunguu maji, karoti vilivyobanikwa na samaki ndani ya oven
Jaribisha mpiko huu wa samaki, ambao ni rahisi sana kuupika, kisha tujuza je, uliupenda upishi huu, pengine tutumie na picha kutuonesha jinsi samaki wako walivyotokea, anwani yetu ni info@menutimetz.com au menutimes@gmail.com
Kutoka jiko la Menu time, LJM anafunza!!
No comments:
Post a Comment