Thursday, August 2

Akili ni nywele kila mtu ana zake - Ubunifu

   Kuna namna nyingi ambazo mwana wa adamu unaweza jipatia huduma zako tofauti na vile tulivyozoea, au niseme kwa kutumia njia mbadala.
   Ili kimiminika kiwe baridi tumezoea kukiweka kwenye jokofu a.k.a fridge ili kipate kupoa, na hii hutumika sana maeneo yenye hali ya hewa ya ujoto mathalani Dar iliyo salama nakadhalika. Kwenye sehemu za baridi niongelee Tanzania mathalani Mufindi, Njombe n.k mara nyingi hawatumii majokofu, kwani tayari kimiminika hicho kinakua na ubaridi kutokana na hali ya hewa ya hapo.
   Sasa basi iwapo huna jokofu haimaanishi huwezi jipatia kimiminika cha baridi, kuna njia mbadala na katika pitapia zetu, mkoa wa Songea kuleee Mbinga, tulipishana na mama mmoja, mjasiriamali ambaye ana duka lake analouzia bidhaa za kila siku za mwananchi akatujuza zaidi.
   Eneo alilopo hakuna umeme na hivyo ametumia njia mbadala kuhakikisha wateja wake wanapata vimiminika baridi kama soda. Aliniambia anachukua chungu na kuweka maji na chupa za soda ambazo bado hazijafunguliwa kwa wingi wa kiasi kama chupa 7 hivi, na kuzilaza ndani ya maji yaliyomo ndani ya mtungi kwa usiku mzima, na asubuhi zinakua na ubaridi mzuri tu wa kumwezesha mnywaji kukata kiu yake.
   Asubuhi huutoa mtungi wake na hivi ndivyo unavyoonekana

   Vyungu hutengenezwa humuhumu Tanzania, na hutumika kwa matumizi ya kupikia, kuhifadhia na leo hii tumejifunza pia kupoozea vimiminika.
   Tujuze ubunifu uliopishana nao ili nasi tuongeze ubunifu na ujuzi ndani ya maisha yetu. Menutime itajitahidi kuwasiliana na watengeneza vyungu ili tupate ujuzi na maarifa zaidi ya vyombo hizi.
   Kutoka Mbinga, Songea menutime inawatembeza.

No comments:

Post a Comment