Saturday, December 8

Vyakula bora kwa aishie na VVU

  Leo tunamalizia kwa kuangalia Umuhimu wa maji, viungo vipi vyaweza kusaidia kuongeza hamu  ya kula na ladha ya chakula, iwapo Rafiq amekosa hamu ya kula, pia tutaona vyakula au vinywaji gani vya kuepukwa na wale Rafiqs waishio na VVU.
  Cha kwanza ni kwamba, Maji ni muhimu sana ndani ya miili yetu, na hii ni kwa kila mmoja wetu bila kujali kama tunaishi na VVU au la. Kusoma zaidi kuhusu umuhimu wa maji mwilini, tafadhali rejea makala yetu iliyotolewa tarehe 20 hadi 22 ya mwezi Septemba, iliyoitwa Umuhimu wa maji mwilini. Itafute kwenye Afya Njema.

  La msingi hakikisha kunywa si chini ya lita mbili za maji kwa siku.
            

   Vinywaji ambavyo vyapaswa kuepukwa yaani kutokutumiwa na Rafiqs waishio na VVU ni pamoja na chai, kahawa, soda na vinywaji vyenye ulevi. Imedhibitishwa kuwa vinywaji venye ulevi hufanya mwili kupoteza maji kwa wingi, hivyo si vyema kutumiwa na Rafiqs waishio na VVU. Kama tulivyosema hapo juu ya kuwa maji ni muhimu mwilini, hivyo ni sahihi kuepuka vile vyanzo vya umalizikaji wa maji mwilini ikiwemo vinywaji vyenye ulevi.

 
    Kuna viungo ambavyo hutia chachu au hamasa ndani ya chakula na kumfanya mlaji kupata hamu ya kula au kuendelea kula iwapo chakula kilimshinda mara ya kwanza. Viungo hivi huweza kupikwa ndani ya mlo au kuliwa wakati wa mlo, itategemeana na mapenzi ya mtumiaji.
  Baadhi ya viungo hivyo ni pamoja na Vitunguu swaumu, tangawizi, papai bichi, madalansi na iliki. Hivi viungo husaidia kwenye kukiyeyusha chakula ukiondoa msaada wa kuongeza hamu ya ulaji chakula.


     Na hapo tumefikia mwisho wa mada hii ya "Vyakula bora kwa aishie na VVU" ambapo tumeona vyakula vya aina mbalimbali ambavyo vitamsaidia Rafiq kuweza kujenga afya yake na kuongeza nguvu mwilini.
   Tunaamini vyakula vya makundi yote vitaweza kupatikana sehemu mbalimbali ili iweze kuleta urahisi wa ununuzi na matumizi.
   Iwapo kuna maoni, swali, ongezeo la mada hii, jisikie huru kuwasiliana nasi kupitia anwani yetu info@menutimetz.com nasi tutazungumza nawe.
    Kutoka timu ya MT, tunasema Tanzania bila Ukimwi Inawezekanika!! Tusiwanyanyapae Rafiqs waishio na VVU, tuwapende, tuwajali na kuwasaidia kwani ni wenzetu.

No comments:

Post a Comment