Thursday, June 30

Menyu ya Asubuhi - Mbagala

Katika pitapita yangu nilikutana na Rafiq anatengeneza vitafunwa vyaitwa Vitumbua. Tayari alikua ameshachanganya na nilimkuta katika steji za mwisho. Ilikua asubuhi kama saa 2, akanieleza kila siku huwa anavipikia hapo hapo na kuuzia hapo hapo. Pembeni kuna meza, viti na chupa ya chai unajisevia, unalipa kisha unasepa.
Vitumbua vina kikaangio chake maalum, na sio kwenye kikaangio cha kawaida. Ule muonekano wake watokana na shape ya kikaangio chake.

Kama nilivyosema nilimkuta tayari keshaanza mapishi, kuna nafasi sehemu moja tu ya kikaangio

Hapa anamimina mchanganyiko kwenye kikaango

Mafuta yanaongezwa kidogo, ili kitumbua kisije kukaukia kwenye kikaango

Kikishaiva upande mmoja, kinageuzwa upande wa pili kiweze kuiva vyema, kisha huepuliwa na kuwekwa kwenye sinia tayari kwa mauzo.

Na kwa shilingi 100/= tu za kitanzania unapata Kitumbua chako, ukishushia na chai , siku inaanza vyema. Vitumbua vyaweza kuliwa muda wowote sio lazma asubuhi tu. Wengine hupenda kuweka kuwa moja ya mlo wa sherehe.
Nilipokwazika mie, ni kutokuwa na kawa au mfuniko flani kuweza kuvitunza katika sehemu salama zaidi. Ila tulizungumza, alikubali kuandaa kijisanduku cha kuuzia vitumbua vyake.

Karibu kutoa maoni yako, tuma barua pepe kupitia menutimes@gmail.com

Menyu ya Asubuhi - Mlimani City

Rafiqs wengine wao hupenda kufungua vinywa vyao na chai ya rangi, kuna wa chai ya maziwa, kuna wale wa Kahawa yenye maziwa, Kahawa nyeusi na aina kadha wa kadha.Yawezekana ni mazoea, au ni hamu uliyoamka nayo, kwamba leo nataka ninywe chai yenye ndimu asubuhi hii au maziwa mgando ilimradi tu vile hamu inapokupeleka.
Rafiqs hawa walikua Mlimani City na waliamua kufungua vinywa vyao kwa Cappuccino, Kahawa nyeusi na vitafunwa. Aliyekua anakunywa Kahawa nyeusi hakuweka sukari ila kitafunwa chake kilikua na sukari mno, binafsi nikahisi basi vikichanganyika kinywani utamu unakua vile anavyotaka.
Kuna wale babu zetu na hata vijana wanakunywaga ile kahawa chunguuuu na kashata mtaani, nawaona kama wanakua wamejiwekea hesabu/ vipimo flani hivi mdomoni, yaani fundo hii na kiasi cha kipande hiki vinaenda kusawazishana mdomoni... Ubunifu katika mlo au???Karibu tuwaone wa Mlimani City...


Rafiq, Iwapo ungependa kutuonesha Kifungua kinywa chako, tuwasiliane kupitia menutimes@gmail.com

Wednesday, June 29

Menyu ya Asubuhi a.k.a Breakfast - Nyumbani

Toka nyumbani kuna siku ambazo binafsi nafungua kinywa na uji wa ulezi. Huu huwa unapikwa na mama mzazi. Yaliyomo humo ndani ni pamoja na Unga wenyewe wa ulezi, maziwa freshi, siagi, mtindi kiaina, basi unakuwa na ladha flani tamu, ngumu kuelezea kidogo.
Waweza upata huu unga wa Ulezi toka kwenye Supermarkets mbalimbali. Huu uji wa ulezi una mapishi tofautitofauti na unanyweka sehemu nyingi sana. Kuna kina mama wanaupika, wanaweka kwenye thermos a.k.a chupa za kuwekea chai/ maji moto, kisha huenda kuuza. unapendwa sana!

Kuna siku ntakujuza namna ya kuupika utokee na utamu naotaka kukueleza. Kwa leo furahia picha yake, Karibu!!


Kikombe kimoja tu chantosha kuanza siku vyema!

Menyu ya Asubuhi a.k.a Breakfast - Tabata

Kifungua kinywa sio lazima ukipatie nyumbani. Popote pale inawezekana, iwe ofisini, mgahawani, nyumbani au kwengineko,cha msingi muda uwe wa asubuhi na uwe ndo mlo wako wa kwanza,ikimaanisha ndio mlo unaofungua kinywa.
Asubuhi moja nilipita mitaa ya Tabata, nikawakuta Rafiqs wakipata kifungua kinywa chao, ndani ya baa moja matata sana.


Hii ni supu ya utumbo. Chuzi halijaongezwa maji wala kiungo chochote. Pilipili, ndimu na chumvi huwekwa pembeni kwa ajili ya kujiongezea ladha kama utapenda.
Menyu hiyo kwa hela taslim za kitanzania shilingi 2,000/= tu unaipata.
Japokuwa hizi sahani zinasaidia kuweka vitu vingi, na zatumika kwa wingi kwenye mabaa na baadhi ya migahawa binafsi sijawahi kuzipenda kabisa. naona kama kubwa sana!! mtazamo wangu tu!!

Kifungua kinywa a.k.a Breakfast

Nilipata bahati ya kutembelea pande kadhaa za Dar Es Salaam, na kushuhudia Rafiqs wakipata kifungua kinywa sehemu tofauti tofauti. Kutoka Mlimani City hadi Tabata. Nilikatiza Mbagala na kwingineko. Ntarejea kukujuza zaidi !!!!

Monday, June 20

Menyu toka kwa Rafiq

Rafiq alipata mualiko pande za Kariakoo - Dar es salaam - Tanzania!!.
Na hii ndio picha ya menyu aliyoandaliwa na Rafiqs zake

Haswa paliponifikisha ni suala zima la ubunifu, kama huna zulia na muda wa menyu umefika, tandika magazeti ambayo ulishayasoma chini na andaa menyu yako, kisha waite rafiqs wakaribie. Mwisho wa siku kinachojalisha ni mwito na namna ya pekee uliyowakumbuka na kuwaandalia.
Menyu imekamilika: Msosi kamili, Tunda, Juisi, Chai, halafu Kachumbari nayoooooooo laaah!! hakika walifurahi!!

Asante sana Vincent Koola kwa kushare nasi picha hii nzuri.

Karibu kushare nasi picha za msosi: aidha umeupika, umepikiwa, umealikwa kula, umejialika au hata umeenda kununua.Piga picha na tutumie picha yako kwetu kupitia anwani yetu ambayo ni menutimes@gmail.com

Menyu toka kwa Rafiq

Toka kwa Rafiq, ametuletea picha  ya Supu aliyokua anakunywa. 
Hakueleza muda gani alikua anainywa kama ni ya kukatia mning'inio a.k.a Hangover au kutuliza njaa.


Mark Andere asante sana bro!! Nimependa chupa hiyo pembeni!!!

Kama una picha ya menyu uliyokula au umepika tafadhali tutumie kupitia menutimes@gmail.com.

Thursday, June 16

Mtwara - Makonde beach Club

Kutoka Mtwara Amani Lyimo ametutumia picha anasema menu hii inapatikana Makonde Beach Club kwa fedha za Kitanzania Sh 10,000/= tu. 


Asante sana Amani!!!

Monday, June 13

Dar es Salaam

Shawarma zapatikana Dar Es salaam sehemu mbalimbali. Zamani kidogo ilinipasa kusubiri mpaka maonesho ya sabasaba ndo niweze kupata kula Shawarma, lakini siku hizi, Victoria, mikocheni, City center na sehemu kadhaa zinapatikana.

Shawarma ni sandwich ya kiarabu ambapo chapati au mkate ya duara laini  hutumiwa kuvingirishwa nyama   (aidha ya mbuzi, kondoo, kuku, ng'ombe au mchanganyiko wa vyote) ndani yake pamoja na vionjo vingine 
Nyama hii huwekwa kwenye jiko maalumu na kuokwa taratibu kwa muda mrefu. Nyama ya nje inapoiva hukwanguliwa na kuacha ya ndani ipate nafasi ya kuiva.
Moja ya sehemu walinionesha kidogo namna wanavyotengeneza........ Karibu!!

  • Hapa Shawarma ipo jikoni inaendelea kuiva taratibu.....,



  •  Na baada ya  dakika 30 Shawarma ikawa imeiva vyema tayari kwa kuliwa.


  • Chapati spesho zinatayarishwa kwa kupashwa moto, maana tayari zinakuwa zilishapikwa:

  • Vipande vya nyama vilivyookwa na kuiva vyema vinawekwa ndani ya chapati iliyofunguliwa:



  • Mchanganyiko mwingine unaongezwa hapa, ambao sikuweza upata wote:


  • Shawarma imefungwa na kuviringishwa ndani ya karatasi laini linalisaidia isidondoke na iwe rahisi kubeba. Kwa yule ambaye angependa kula pale pale ipo tayari kwa kuliwa:


  • Kwa atakaye penda kuibeba a.k.a Take away basi wanaifunga vyema namna hiyo:


Sunday, June 12

Kigoma

Menyu ya mwisho Kigoma, aliagizia Victor, tulikua Amarula bar. Ndizi Mzuzu na kuku. Kachumbari kwa pembeni !!!

Kigoma

Pande za Ilagala bado nipo, na kama tunavyojua dagaa ndo zinapotoka Kigoma.
Hapa nilikutana na wajasiriamali wameanika dagaa wakizikausha tayari kwa mauzo.



Kwa karibu zaidi, Dagaa wa kigoma:

Kigoma

Nilifika Ilagala, huku nilikutana na marafiki wengi sana. Nilibahatika kuona kivuko chao.

Hapa upande mmoja umeng'oka hivyo wamebuni kuweka gogo ili kurahisisha na kusababisha magari, baiskeli na mizigo mingine iweze kuingia kwa urahisi

Kaka analengesha baiskeli yenye mzigo iweze kupita kwa urahisi na usahihi kwenye gogo.

Pembeni kipande cha chuma kilichong'oka kimeegeshwa. Naamini wahusika wapo mbioni kurekebisha kivuko hiki.

Kigoma

Ya nne ilikua ndizi mzuzu na kuku wa kienyeji, Eneo limenitoka kidogo ila nikipakumbuka ntawahabarisha:

Kigoma

Menu ya tatu ilitokea Hotelini, Ukweli tuliagiza Chicken Pizza. Na hii ndio tuliyopata:

Kigoma

Hoteli niliyofikia yaitwa Lake Tanganyika Hotel, Kigoma.
Pazuri mno panavutia, na picha hizi nakuonesha mandhari kadhaa ya Hoteli hiyo:

  • Kutoka baraza la chumba changu, hii ndo mandhari unayoipata


  • Mandhari ya maeneo mengine ya Hotel:




Kigoma

Ya pili ilikua ni mchemsho wa kuku wa kienyeji wapatikana Kizota bar. Unachanganywa na ndizi tamu muno

Kigoma

Nilipata kula sehemu mbalimbali, wenyeji wangu kina Victor, Mashine, Robert a.k.a Kagame,Ben, Mike moja, Nobert, Oliver a.k.a Chalii ya A town, walikuwa wakinipeleka.
Karibu uone menu za Kigoma:

Ya kwanza, Kitimoto rosti yapatikana Amarula bar, matata sana ukiila na ugali!!


Friday, June 10

Kigoma

Ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kigoma tulipokelewa na salamu zifuatazo:


Tulitua salama salimini tukakutana na Tangazo hili: 


Na hapa ndo unapochukulia m(i)zigo w(y)ako tayari kwa kuingia Kigoma.


Ukweli wapaswa kusemwa, mandhari ya Uwanja wa ndege wa Kigoma ni safi na unapendeza mno. Bustani zinaangaliwa vyema. Hongereni sana !!

Safari ya Kigoma

Namshukuru Mwenyezi Mungu nimerejea salama salimini toka safari ya Kigoma. Shukrani ziwafikie wenyeji wangu na marafiq wapya niliokutana nao kwa kunitembeza vyema mkoa wa Kigoma.

Ndege iliyotutoa Mwanza mpaka Kigoma ni hii hapa. Safari ilikua nzuri tu, japo unatahadharishwa kutokunywa sana au kula kabla ya safari maana hamna sehemu ya kujificha na kupiga simu wala kutuma sms ndani humo.



Tukiwa njiani, baadhi ya mandhari nilizoweza kupiga picha ni pamoja ni hizi:
Picha ya Hotel ya Malaika iliyoko Mwanza


Gurudumu la ndege yetu



Tunawasili kigoma


Usukani wa bwana Rubani ..

Karibuni Kigoma