Tuesday, May 14

Upishi wa chapati maji a.k.a pancakes


  Leo tunafundishana upishi wa chapati maji a.k.a pancakes. Kila mmoja wetu ana namna yake ya kupika kutokana na kupenda chapati maji hiyo itokee na ladha gani. Leo Menu Time katika upishi huu tunatumia viungo tofauti kidogo katika kuongeza ladha kwa mlaji. Karibuni!!

Mahitaji:
  • Unga wa ngano - kikombe kimoja na nusu
  • Maziwa kikombe kimoja
  • Yai moja
  • Blue band kiasi (kwa ajili ya kukaangia chapati maji zako)
  • Chumvi- nusu kijiko cha chai
  • Sukari - kijiko kimoja cha chai
  • Asali kijiko kimoja cha chai
  • Unga wa Cocoa kijiko kimoja cha chai
  • Kitunguu maji nusu
Hatua:
  • Chukua chombo kikubwa cha kutosha kuchanganya viungo vyako. Weka unga, pamoja na maziwa na yai kisha koroga kwa pamoja. Hakikisha vimekorogeka vyema, kisha katakata vitunguu maji katika vipande vidogo vidogo sana, kisha changanya na mchanganyiko wako. Ongeza chumvi, sukari, unga wa cocoa pamoja na asali kisha koroga mchanganyiko wako kwa kutumia mwiko wa mbao hadi mchanganyiko wako uwe umechanganyika vyema na hauna mabongebonge.
  • Mchanganyiko utaonekana kama hapo chini kwenye picha
  •  Weka kikaangio kwenye moto, kisha acha kipate joto na ongeza kijipande cha blue band kidogo ili kuzuia chapati maji isigande kwenye kikaangio
  • Weka mchanganyiko wa chapati maji kwa kupima, vijiko viwili vya kupakilia, kisha tandaza kwenye kikaangio ili kutengeneza umbo la duara
  • Acha chapati maji ipate kuiva vyema kwa kuiacha ikauke upande wa juu kabla ya kuigeuza, kama inavyoonekana kwenye picha
 
  • Geuza chapati maji yako na kuiacha ipate kuiva vyema upande wa pili, kuwa makini ili kuzuia chapati maji kuungua lakini hakikisha imeiva vyema. Utakapoigeuza, upande wa mwanzo utaonekana kama ilivyo kwenye picha hapo chini
  • Baada ya kuhakikisha upande wa chini/ pili nao umeiva, epua chapati maji yako tayari kwa kuliwa na walaji wako

Chapati maji yaweza kuliwa na kitu chochote iwe ni chai, maziwa, mboga yeyote, soda au hata hivyo hivyo, ikitegemea na umejiandaaje na mlo wako.
   Kuna wanaokula kama kifungua kinywa, kuna wale wa cha mchana au usiku na wengine kama bites, inategemea na muda gani ungependa kupata mlo wako wa chapati maji

   Mpaka hapo tunakua tumefika mwisho wa mapishi ya chapati maji a.k.a pancakes yenye maziwa n.k.
   Kushare nasi namna ya kupika menu yoyote, wasiliana nasi kupitia barua pepe menutimes@gmail.com

No comments:

Post a Comment