Wednesday, March 13

Mapishi ya ngisi rosti a.k.a calamari rost

   Chakula cha majini a.k.a sea food, ni moja ya vyakula navipenda mno. Mara nyingi inakua rahisi kuvipata kutoka mgahawani, kitaani, restaurants na kwingineko. Pengine labda ni kwasababu muda unakosekana wa kufuata hawa viumbe kule feri. Pia hata kununua kwenye maduka makubwa a.k.a supermarkets nakuwa najisahau, hivyo nkishikwa na hamu ya kula sea food nawahi kwenye mgahawa ambao najua unapika vyema sea food na kutimiza kiu yangu.
   Wikiendi iliyopita, siku ya Jumapili, nilipika ngisi na vinginevyo vitakavyoonekana kwenye sahani. Nataka kushare na wewe nilivyoipika hiyo mboga ya ngisi ili na wewe ujaribu.

Mahitaji:
  • Ngisi - nusu kilo
  • Chumvi - kiasi
  • Pilipili manga- kiasi
  • Vinegar
  • Tangawizi - kiasi
  • Kitunguu swaumu - kiasi
  • Olive oil - kiasi
  • Karoti - kimoja
  • Pilipili hoho - kimoja
  • Kitunguu maji - kimoja
  • Ndimu - moja
  • Pilipili kichaa - moja
( Kiasi - inamaanisha kutokana na mahitaji yako na upendavyo)

Hatua:
  • Tayarisha mahitaji yako kwa, kutwanga pilipili manga, tangawizi, kitunguu swaumu. Lakini vitwange tofauti tofauti na kuviweka tofauti
  • Chukua chombo weka ngisi wako, kisha ongeza chumvi kiasi, pilipili manga kiasi, tangawizi kiasi, kitunguu swaumu kiasi, nusu ndimu na vinegar. Changanya mchanganyiko huo kisha vifunike viache viungo vikolee vyema ndani ya ngisi kwa kama nusu saa
  • Katakata karoti, vitunguu maji pamoja na pilipili hoho katika umbo la urefu ili kufanana na urefu wa ngisi kisha weka pembeni
  • Chukua mchanganyiko wa ngisi na viungo bandika jikoni na ongeza maji kidogo ili kuruhusu ngisi kuiva taratibu. Endelea kuongeza maji kila yanapokauka kwa muda wa kama dakika 15 kisha onja ngisi wako kama wameanza kuiva 
  • Epua ngisi, na weka sufuria lingine jikoni. Weka mafuta kiasi na yaache yakaangike kiasi, kisha ongeza chumvi kiasi na vitunguu maji. Vitunguu maji vikishaiva na kubadilika rangi, ongeza vipande vya karoti na pilipili hoho na pilipili kichaa moja isiyokatwa, pamoja na viungo vingine kama pilipili manga, kitunguu swaumu, tangawizi (iwapo utapenda kuongeza, maana tulishavichemshia kwenye ngisi)
  • Baada ya mchanganyiko wa karoti, vitunguu maji, pilipili hoho na viungo kuiva na  kuchanganyika kama kwa dk 5 hivi, weka ngisi walioshachemka, kisha koroga vyema na acha viive kwa pamoja
  • Koroga vyema ngisi wako, kisha ongeza blue band kidogo sana kwa ajili ya kuongeza ladha, koroga na malizia kwa kuweka curry powder, na baada ya kama dakika 2 mboga yako itakua tayari kwa kupakuliwa na kuliwa.
     Sasa waweza kula na ugali, wali, viazi au kingine chochote kutokana na maamuzi yako. Jumapili sisi tulikula na wali mweupe, mchicha pamoja na salad ya mahindi machanga
Ushuhuda ni huu hapa chini

    
   Jaribisha pishi hilo, kisha tujuza kupitia menutimes@gmail.com ili nasi tuone ushuhuda wa menu yako.
   Kutoka jikoni kwa Menu time, LJM naarifu.

No comments:

Post a Comment